Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, awamu ya pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Usomaji wa Qur’ani Tukufu imeanza mjini Islamabad, kwa juhudi za Wizara ya Masuala ya Kidini na Uratibu baina ya Madhehebu ya Pakistan, huku ikishirikisha wasomaji mahiri wa Qur’ani kutoka nchi 32 duniani.
Mashindano hayo ya kimataifa yanayodumu kwa siku tatu, ambayo yataendelea hadi tarehe 26 Novemba, yanafanyika kwa ushiriki wa wasomaji kutoka nchi mbalimbali.
Sardar Muhammad Yusuf, Waziri Mshauri wa Masuala ya Kidini na Uratibu baina ya Madhehebu wa Pakistan, katika hotuba yake, aliwakaribisha wasomaji wa Qur’ani na wageni kutoka nje ya nchi, akiwashukuru kwa kushiriki kwao nchini Pakistan. Aidha, alieleza kuwa mkusanyiko huo wa Qur’ani ni fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano baina ya mataifa ya Kiislamu. Pia aliwatakia washiriki wote mafanikio.
Katika awamu hii ya mashindano, wasomaji wa Qur’ani wanaoshiriki wataonesha uwezo wao kupitia usomaji wenye mvuto na ufundi, hususan katika kuzingatia kanuni za Tajwidi, matamshi sahihi ya herufi, usahihi wa kutamka maneno na mbinu mbalimbali za usomaji wa Qur’ani Tukufu.

Mbali na kuibua na kuwatambulisha vipaji mahiri katika nyanja ya Qur’ani, mashindano haya pia yanatoa mazingira mwafaka ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha mawasiliano baina ya wasomaji wa Qur’ani pamoja na watendaji wa shughuli za Qur’ani kutoka nchi mbalimbali.
Kufanyika tukio hili la kimataifa kunahesabiwa kuwa hatua muhimu katika kueneza utamaduni wa Qur’ani, kupanua mafundisho ya Kiislamu na kuimarisha uhusiano wa kidini na kiutamaduni baina ya nchi za Kiislamu.
Vilevile, programu za aina hii zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kuimarisha uhusiano wao na Qur’ani Tukufu, pamoja na kujitahidi zaidi kujifunza usomaji, kuhifadhi na kusoma kwa kuzingatia kanuni za Tajwidi za Kitabu hiki kitukufu.
Inafaa kutajwa kuwa awamu ya pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Usomaji wa Qur’ani Tukufu inafanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Novemba 2026, mjini Islamabad, na itahitimishwa siku ya tarehe 26 Novemba.
Maoni yako